Muundo wa Muungano: Serikali Tatu, Moja, Mbili? Zote!
Zitto Kabwe
Mwalimu Azaveli Lwaitama ni mwalimu na mlezi wangu nje ya darasa.
Alipokuwa Katibu wa Umoja wa Wanataaluma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
mimi nilikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Idara ya Uchumi. Nilikuwa
nashinda kwenye Ofisi ya UDASA tukijadiliana kuhusu Umajumui wa Afrika
(Pan-Africanism), Ujamaa na harakati za kulinda haki za watu. Ilikuwa ni
nadra kwa mwanafunzi wa uchumi kuwa karibu na mwalimu wa lugha na
mnadharia mkubwa. Wanafunzi wa uchumi tulikuwa tunajidai na kujivuna.
Tulikuwa tunajiona bora sana maana darasa letu halikuwa linazidi watu 40
na kwa kweli wote hawamalizi. Darasa langu tulimaliza wanafunzi 25 tu
kati ya 40 tulioanza. Mwalimu Lwaitama ni mpenzi mkubwa wa Muungano kama
nilivyo mimi. Tumeapa kuulinda kwa namna yeyote ile. Yeye alikuwa
mhafidhina (conservative) sana akitaka Muungano wa muundo huu aliouacha
Mwalimu Nyerere. Mimi nataka kuulinda kwa kuufanyia marekebisho makubwa
sana ya kimuundo. Hatukuwa tunakubaliana.
Wiki iliyopita
Mwalimu Lwaitama kaandika kuhusu muundo wa Muungano katika makala zake
za kila wiki katika gazeti la kimombo la The Citizen. Amebadili msimamo.
Ameona sasa muundo wa Muungano ulivyo sio endelevu. Ametoa mapendekezo
niliyoyatoa siku za nyuma katika mazungumzo yetu ingawa yeye bado
anayasema kwa shingo upande. Lwaitama sasa anataka Serikali mbili
zilizonyumbuliwa. Anapendekeza Waziri Mkuu wa Muungano mwenye nguvu za
za kitendaji. Nampongeza kwa kuboresha mawazo yake.
Hata hivyo
bado Mwalimu wangu na Watanzania wengi wamejikita katika mjadala wa
Serikali ngapi. Idadi ya Serikali inaonekana kama ndio dawa ya kero za
Muungano. Ni kweli Wazanzibari wanataka uhuru zaidi na wengine hawataki
kabisa Muungano. Unawalalia. Unawanyima uhuru wa kuamua baadhi ya mambo
yao na japo halisemwi unawanyima wanasiasa wa Zanzibar mamlaka ya
masuala mengine ambayo yangewafanya wajilimbikizie madaraka.
Huku bara napo kuna watu, tena wanaongezeka kwa kasi kweli kweli,
wakitaka Tanganyika yao. Tena wengi vijana. Demografia zetu zinaonyesha
kwamba Watanganyika waliozaliwa Tanganyika ni takribani asilimia 12 tu
ya Watanzania. Asilimia 70 ya Watanzania wamezaliwa wakati Muungano
umeshasherehekea miaka 15 ya kuzaliwa kwake. Lakini wanataka Tanganyika
yao. Wamechoshwa na kelele za Wazanzibari. Hawawataki Wazanzibari kujaa
kwenye Bunge la Muungano wakati wapo kiduchu sana. Wanasiasa nao, japo
hawasemi waziwazi wanataka wawe na mamlaka zaidi bila kulazimika
kushauriana na wanasiasa wa Zanzibar. Linapokuja suala la wagombea Urais
ndio kabisa wanakereka kutafuta mgombea mwenza kutoka Zanzibar.
Wachambuzi wa historia za kisiasa siku wakiamua kufanya tafiti watachoka
na roho zao watakapoona aina za wagombea wenza ambao wagombea Urais
huteua, hasa kutoka sisi vyama vya upinzani.
Kimsingi idadi ya
wapinga Muungano inazidi kuongezeka siku hata siku. Ukiwauliza kwa nini
hawataki Muungano wanasema aah, basi tu. Kama ni Mzanzibari atasema
Tanganyika wanatutawala. Kama ni Mtanganyika atasema Wazanzibari
wamezidi kelele, tunataka Tanganyika yetu. Sisi ‘Unionists’
(Wanamuungano) nao hatuna majibu ya kuridhisha sana na ya kukonga nyoyo.
Isipokuwa tu, Muungano huu ni wa aina yake Afrika na Duniani. Ni alama
pekee ya kuonyesha Mwafrika kupinga mipaka ya kikoloni. Sasa hili
haliwaingii kichwani ‘secessionists’ (Wanautengano) na hatuna la
kuwasaidia. Lakini ni lazima tuurekebishe Muungano huu. Ulivyo sasa
utavunjika tu. Kuulinda Muungano ni kuufanyia marekebisho makubwa.
Mwalimu Lwaitama kaliona hilo. Pendekezo lake liboreshwe sasa. Sio
rahisi sana.
Sasa tufanyeje? Serikali moja itaimeza Zanzibar.
Serikali Tatu ni gharama kuendesha na Serikali mbili zimeimeza
Tanganyika na watu wanataka Tanganyika yao na zinainyima uhuru Zanzibar
na watu wanataka wawe huru zaidi. Mfumo wa Serikali ngapi na kadhalika
ni moja ya mikakati ya wanasiasa katika kusaka vyeo. Sisemi sio halali
kujadili lakini kiukweli mfumo gani wa Muungano hautaongeza fungu la
dagaa kwa mwananchi wa Kagongo au sinia la ubwabwa kwa mwananchi wa
Mkanyageni. Waingereza wana msemo ‘unataka kula keki yako na kubaki
nayo’, basi tuwe na Serikali zote.
Nimeanza na Mwalimu Azaveli
Lwaitama. Naboresha hoja yake kwa kurudia niliyowahi kuyasema huko nyuma
kuhusu muundo wa Muungano. Tuwe na Dola Moja tu. Ndio, Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na wala sio Shirikisho la Tanzania (kwanza
litatuondoa kwenye kiti chetu kule Umoja wa Mataifa maana kwa jina letu
sisi tunakaa katikati ya Uingereza na Marekani. Katikakati ya mabwana
wakubwa, labda ndio maana wanatupa misaada sana, unajuaje?). Tuwe na
Rais mmoja tu mwenye mamlaka kamili ya Asasi za Dola – Mambo ya Nje,
Ulinzi na Usalama, Uhamiaji, Sera za Fedha na jukumu la jumla la
kusimamia ustawi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Achaguliwe na
Watanzania wote wa pande zote mbili za Muungano kwa kupata zaidi ya nusu
ya kura za pande zote za Muungano. Tuachane na mambo ya Mgombea Mwenza.
Tumejaribu tumeona hana maana zaidi ya kutembea na mikasi tu.
Zanzibar iwe na Waziri Mkuu Mtendaji kwa masuala yote ambayo sio ya
Muungano. Tanganyika iwe na Waziri Mkuu Mtendaji kwa masuala yote ambayo
sio ya Muungano. Hawa watateuliwa na Rais wa Muungano kutoka chama
chenye Wawakilishi wengi katika Baraza la Wawakilishi Tanganyika na
Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Wote watakuwa ni Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano kwa utaratibu kwamba iwapo Rais anatoka Zanzibar,
basi Waziri Mkuu wa Tanganyika atakuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na wa
Zanzibar atakuwa Makamu wa Pili wa Rais. Kule kule kwenye misingi haswa
ya Muungano. Hawa wataongoza Mabaraza yao ya Mawaziri na watakuwa na
nguvu ya kuteua na kufukuza Mawaziri wanavyotaka. Hawatakuwa Wabunge
katika Bunge la Muungano.
Bunge la Muungano litakuwa dogo lenye
Wajumbe wasiozidi 101 pamoja na Rais wa Bunge la Muungano. Wabunge wa
Muungano watatoka kwenye mikoa (au Majimbo kama sera ya Majimbo
itakubalika). Kwa utaratibu wa sasa kila mkoa utachagua wabunge 2 mmoja
mwanamke mmoja mwanaume kwenda Bunge la Muungano. Wajumbe wa Ziada
watatokana na uwiano wa kura ambazo kila chama kimepata kwenye kura za
Rais wa Muungano. Idadi hii yaweza kupunguzwa na hata kuwa na Wabunge 51
tu akiwemo Rais wa Bunge la Muungano ambapo kwa mikoa ya sasa kila mkoa
utachagua Mbunge 1 na wengine watokane na uwiano. Rais wa masuala ya
Muungano atakuwa Mkuu wa Shughuli za Serikali katika Bunge la Muungano
na Rais kwa mwaka mara moja atahutubia Baraza la Taifa (Wabunge wa Bunge
la Muungano na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka kila upande wa
Muungano). Wazungu wanaita hotuba hii ‘State of the Union’ (Hali ya
Taifa) na wengine huita ‘Queen’s Speech’ (Hotuba ya Malkia).
Mkuu wa nchi mmoja, Dola moja ya Jamhuri ya Muungano. Serikali mbili na
kila upande una Serikali yake yenye mamlaka kamili ya maisha ya watu wao
ya kila siku. Haya matatu pamoja na Serikali ndogo ya Muungano. Lakini
tutakuwa tumepata kila kitu labda. Wenye kutaka Uhuru mpaka Zanzibar
watapata. Wenye kutaka Tanganyika watapata na wenye kutaka Muungano kama
Dola yenye nguvu watapata
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment