Wednesday, February 26, 2014

MWALIMU NYERERE ALIVYOWACHAPA VIBOKO WANAFUNZI WA CHUO KISHA KUKIRI NA KUWAOMBA RADHI

JE WAJUA?

MWANAFUNZI WA CHUO KIKUU WILFRED MWABULAMBO ALICHARAZWA VIBOKO KWA KUMGOMEA RAIS NYERERE!

Wanafunzi wanapogoma au kufanya maandamano, dola hujibu mapigo kwa njia anuai. Ipo mifano ya wanafunzi waliosimamisha au kufukuzwa chuo, kuswekwa korokoroni na kuchukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu kwa kujihusisha kwao na maandamano yasiyo na kibali cha dola.

Ni vigumu mtu kuamini kwamba kati ya hatua zinazoweza kuchukuliwa kuwadhibiti wanafunzi wa chuo kikuu wanaoonekana kuwa watukutu ni kuwaadabisha kwa bakora! Amini usiamini, hapa nchini imewahi kufika pahala serikali, tena chini ya Mwalimu Nyerere kuwatandika viboko wanafunzi waliokosa utiifu kwa viongozi wa serikali.

Mfano wa hili ni kwenye mgomo wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam dhidi ya tamko la uhuru wa walowezi wa Zimbabwe (Unilateral Declaration of Independence-UDI) la mwaka 1965 chini ya Ian Smith.

Ikumbukwe kuwa baada ya Ian Smith na genge lake la walowezi kujitangazia uhuru na kutwaa mamlaka ya kuiongoza Rhodesia ya Kusini (Sasa Zimbabwe), Umoja wa Afrika uliitisha kikao cha dharura , ambapo viongozi wa nchi za Kiafrika waliafikiana kwa kauli moja kuipa shinikizo Uingereza (Waliokuwa wakoloni wa Rhodesia ya Kusini kabla ya kuwaachia walowezi) kubatilisha utawala wa Smith na kuukabidhi uhuru kwa wazalendo.

Azimio la Umoja wa Nchi Huru za Afrika liliweka bayana kwamba kama Uingereza haikutekeleza matakwa hayo ifikapo 15 Disemba 1965 basi nchi zote za Kiafrika zingefuta mahusiano ya kidiplomasia na nchi hiyo.

Uingereza ilipochelea kutekeleza azimio la OAU, Tanzania ilikuwa kati ya nchi za mwanzo kabisa za Kiafrika kufanya uamuzi mzito wa kuvunja mahusiano ya kidiplomasia na Uingereza. Kwenye hotuba yake Bungeni kuhusu suala hili, Mwalimu Nyerere aliweka wazi msimamo wa Tanzania. “Sera za Tanzania na Afrika kuhusiana na suala la Rhodesia ya Kusini mara zote zimekuwa na zitaendelea kuwa na lengo moja tu. Lengo hilo lilikuwa na litaendelea kuwa kupatikana kwa uhuru wa wengi. Kuhusu hili, kila hatua tuliyochukua na kila hotuba tuliyotoa vimelenga kulifanikisha lengo hilo. Hatuna zaidi ya hilo” alisema Mwalimu.

Kwa upande wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama yalivyofanya makundi mbalimbali barani Afrika, wao waliamua kufanya maandamano makubwa kuipinga serikali ya kimabavu ya UDI chini ya Ian Smith ili kuonyesha mshikamano na wapigania uhuru wa Zimbabwe.

Joseph Sinde Warioba aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Wanafunzi Tanzania (National Union of Tanzania Students ) na mmoja wa vinara wa mgomo huo wa mwaka 1965 anatujuza yaliyotokea; “Walowezi wa Zimbabwe walipojitangazia uhuru tuliamua kufanya maandamano kwenye mitaa ya jiji la Dar es Salaam bila kibali. Mwalimu aliagiza tukamatwe na wengi tuliwekwa mahabusu makao makuu ya polisi. Baadaye tulipelekwa Ikulu kuonana naye”.

“Kwenye mkutano wetu alitueleza kwa upole kwamba hatukukamatwa kwa sababu ya kuipinga serikali ya Walowezi wa Zimbabwe bali ni kwa sababu tumevunja sheria kwa kuandamana bila kibali na kwamba tumefanya uharibifu”
“Alisema hakuna hatua zaidi zitazochukuliwa dhidi yetu lakini akatutaka tuiombe msamaha serikali ya Uingereza kwa uharibifu wa mali tulioufanya (Wanafunzi waandamanaji walikwenda ubalozi wa Uingereza na kuharibu mali za ubalozi).

Alisema kuomba msamaha ni utaratibu uliopaswa kutekelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje lakini kwa sababu kwa wakati huo yeye aliishikilia nafasi hiyo, angeomba msamaha, ingetafsiriwa kwamba ni Rais aliyeomba msamaha na si Waziri wa Mambo ya Nje. Hivyo, akatutaka tuombe msamaha kwa niaba yake”

“Baada ya hapo Mwalimu akauliza kama yupo mwenye pingamizi. Mwanafunzi mmoja akasema kwamba analo pingamizi na papohapo Mwalimu akamuamuru kamishna wa polisi amchukue na kumcharaza bakora sita. Ni katika hatua hiyo tuligundua kwamba alikuwa na hasira na sisi. Mazungumzo yote yale ya upole yalikuwa ni njia ya kuficha hasira zake dhidi ya tulichokifanya”

“Baadaye Mwalimu alimuita tena Ikulu yule kijana aliyecharazwa bakora na kumfafanulia kwamba alikuwa ametenda yale kutokana na msukumo wa hasira. Alisema alikuwa ametenda kwa misingi ya ualimu”

“Kama tulivyo wengi, Mwalimu aliweza kupandwa na hasira na kufanya makosa. Lakini moja ya sifa zake ilikuwa ni kwamba hakuona soni kuyakubali mapungufu yake”.

Kijana aliyecharazwa bakora alikuwa ni Wilfred N. J. Mwabulambo. Yeye na Jaji Joseph Warioba, miaka kadhaa baadaye walikuja kuwa viongozi wakubwa serikalini. Wilfred Mwabulambo ambaye sasa ni marehemu amewahi kushika nafasi mbalimbali za Uongozi, zikiwemo ukatibu mkuu kwenye Wizara mbalimbali na pia kuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Jaji Joseph Sinde Warioba ambaye sasa ni mwenyekiti wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Katiba mpya amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais.

Pichani ni Rais Nyerere akiwa na Wilfred Mwabulambo, Picha hii inatajwa kupigwa mwanzoni mwa miaka ya 90 wakati Mwabulambo akiwa Kiongozi Serikalini. Picha na Maelezo husika ni kwa Hisani ya Ndugu Ado Shaibu Ado wa Watanzania Mashuhuri.

Kwa mengi mengine zaidi usiyoyajua kuhusu Tanzania LIKE Ukurasa wetu wa WATANZANIA MASHUHURI ili Upate kujifunza zaidi

No comments :

Post a Comment

 
Copyright © 2013. BongoAfrica - All Rights Reserved.