Wednesday, November 27, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.

‘TANGAZO RASMI LA WAPIGANIA DEMOKRASIA ‘WAUASI’

UTANGULIZI
Katika Tangazo hili yamezingatiwa mambo matano (5)
(1)   Dhana ya Ukabila ndani ya Chadema
(2)   Kuhusu kutonywa.
(3)   Hekaya feki ya kimangimeza
(4)   Dhana ya ughaidi ndani ya chama
(5)   Msimamo wa wapigania Demokrasia wanaoitwa dhidi ya wahafidhina na watiifu wao

Ndugu Wanahabari,
Leo ni siku mpya katika historia ya siasa za vyama vya upinzani Tanzania,
Siasa za upinzani Tanzania zimekuwa zenye kuendeshwa na kuamuriwa na wanaodhani wanamamlaka kuliko mifumo ya uanzishwaji wake,
Nasema ni siku mpya kwa sababu kuu mbili :-
Mosi, ni kwa sababu ya mkakati tulionao na tunaoenda kuutekeleza ili kuziondoa kwenye mwenendo wa uendeshawaji wa kiimla na usanii.
Pili, ni siku mpya kwa sababu leo tutaanza aina mpya ya kushughulika na matatizo ya chama kwa mfimo mpya tofauti na ilivyozoeleka ambayo huwa haizai matunda,
Mimi ninaeongea nanyi naitwa Nyakarungu Grayson mwenye historia ndefu ingawa sio ndefu sana ndani ya chama lakini ni ndefu kabla ya Mzee slaa kujulikana, kabla Zitto kuwa Mbunge, kabla ya Helkopita kuonekana kwenye anga la siasa za Tanzania, kwa ufupi ni kabla ya Chadema kuwa maaurufu kama kilivyo sasa.
Nimetumikia chama tangu mwaka 2005 kama volunteer kwenye idara ya uenezi kutunga na kuimba baadhi ya nyimbo za chama na baadae nilibuni falsafa ya ‘WASHA TAA MCHANA’ iliyovuta wengi kabla ya kuzimwa na wahafidhina kwa sababu za makubaliano walizotaka ambazo kimisingi sikuwa tayari kuzikubali.
Historia yangu ndani ya chama inaaksi maumivu niliyonayo kila ninaposikia habari za upotoshaji juu ya watu wenye kupigania ukweli na misingi ndani ya chama.

Ndugu Wanahabari,
Katika chama cha siasa kuna mfumo wa uendeshaji na taratibu zake kama ilivyo ndani ya chadema, kila taasisi inakuwa na katiba pamoja na kanuni zake za kuendeshea mambo yake,
Hata chadema tunayo katiba na kanuni hizo tena zimeainishwa kitaalam na kiuweledi sana.
Lakini ndugu zangu, unaweza kuwa na kanuni hizo au katiba ya aina Fulani nzuri lakini ukakosa msimamiaji mzuri mwenye utashi chanya wenye nia chanya, matokeo yake utapata mivurugano isiyo na tija wala afya kwa taasisi,
Utashi wa kiongozi ndio huifanya taasisi pamoja na kuwa na kanuni nzuri au mbaya ionekane ni taasisi ya aina gani,
Tukirejea uongozi wa Mwalimu Nyerere aliongoza nchi kwa katiba hii tuliyonayo ingawa imekuwa ikifanyiwa marekebisho lakini tunapata historia ya uongozi mzuri wa Mwalimu katikati ya katiba ambayo leo tunaisema kuwa ndiyo inawapa mwanya viongozi wetu kuiba na kufanya ufisadi, huku tukisahau swala la utashi
Chadema kinajitambulisha kwa umma kama chama chenye malengo na nia ya kutwaa dola wakati wowote, kikitumia mbinu za aina mbalimbali kwenye jamii kikionyesha kina uchungu na wala rushwa, mafisadi na walanguzi, kikihubiri demokrasia majukwaani na kinalilia uwazi wa serikali katika uendeshwaji wa mambo yahusuyo nchi.
Lakini kinachosikitisha ni kuona chadema kinashindwa kuonyesha mfano ndani yake chenyewe,
Kila anaethubutu kuhoji juu ya matumizi ya rasilimali za chama au pesa za chama au mgawanyo wa rasilmali mtu huyo huitwa msaliti au ametumwa na chama tawala,
Viongozi wetu wa chadema wanaohoji serikali na matumizi ya pesa wakitaka uwazi na usawa leo wanataka kutonywa mapema ili wafanye marekebisho ya kuficha uovu wa matumizi ya pesa?
Zitto kama kiongozi anaejipambanua asingeweza kuwatonya ili wafiche uchafu huu huku akitengeneza nafasi ya kuumiza vyama vingine, hii ni dalili ya udikiteta.
Na kwa sababu aligusa mkia wa Mfalme wa NGE lazima ang’atwe,
Tujiulize ni kwanini Zitto alishambuliwa sana na viongozi wa chama baada ya yeye kutoa msimamo na maazimio ya kamati ya PAC?
Walimshambulia yeye binafsi bila kujali kuwa yeye alitangaza maazimio ya kamati na hayakuwa maoni wala maamuzi yake binafsi, lakini utagundua zaidi usanii wa viongiz hawa pindi wanapotaka nafasi Fulani, Mh, Tundu Lissu alipojibiwa na Rais juu ya matamshi yake akiwakilisha kambi ya upinzani viongozi wa chadema walianza kumshambulia na kumkosoa Rais kuwa amemshambulia Msemaji wa kambi ya upinzani kwa kazi aliyotumwa na kambi na kuwa hayakuwa maneno yake binafsi, lakini kwa Zitto walisahau wakaelekeza lawana na matusi kadhaa kwake bila kukumbuka wanachokifanya walikilaumu jana yake kwa Rais kumsema Tundu Lissu.
Tabia hii imelelewa sana, imevumiliwa sana, imewaua wengi kisiasa, imewaneemesha wengi kimaslahi yao.
Ilianza kwa marehemu Chacha Wangwe alipohoji mgawanyo wa ruzuku mikoani akazushiwa kuwa ametumwa na ccm eti yeye ni rafiki wa Rostamu Azizi huku chama kikisahau aliyekuwa mke wa katibu mkuu wa chadema mama Rose Kamili alikuwa Diwani wa kuchaguliwa wa chama tawala kabla hajahamia chadema mwaka 2010, Marehemu Chacha Wangwe alipohoji uhalali wa Mzee Slaa kuwa Katibu Mkuu wa Chadema huku akimiliki mke ambaye ni diwani wa ccm tuhuma dhidi yake na urafiki wake kwa Rostamu zilikoma.
Ndugu Wanahabari,
Tabia hii ikaota mizizi ikamea na sasa inataka kutoa matunda ambayo tunaenda kuyateketeza kwa moto.
Alifuata kafulila alipohoji juu ya pesa zinazodaiwa na Mwenyekiti Mbowe zilizokuwa za receipt za kughushi nae aliondolewa kwenye nafasi yake kinyamela kwa kuitwa sisimizi asiyeweza kung’ata.
Kama vile haitoshi tabia hii ikazaa watoto wanaofanya kazi ya kubuni na kandika HEKAYA FEKI na kuzisambaza kwa umma maana chama kinaamini katika nguvu ya umma.(huu ni upotoshwaji wa falsafa ya chama)
Sakata linaloendelea sasa dhidi ya Zitto Kabwe na Kitila Mkumbo ni mwendelezo wa tabia hii ya kuziba midomo watu wanaohoji mambo ya fedha na matumizi yake.
Hofu ya wahafidhina juu ya uchaguzi wa chama inatokana na kuwa wanajua majeruhi wako wengi wametulia wakingojea uchaguzi wa chama ili wafanye mabadiliko ya chama.
Chama lazima kirudi kwa wanachama kitoke mikono ya wahafidhina kiwe chama cha wananchama.
Wanachama wamevumilia, wameumizwa na wanaishi na makovu yanayotanushwa kila kukicha  wakingojea pengine mabadiliko ya mfumo ndani ya chama yanaweza yakapatikana.
Ndugu Wanahabari,
Mabadiliko hayo hayapo wala hayatatokea kwa njia hizi tuzisubiriazo za uchaguzi huku watu wanaosimamia ukweli na uwajibikaji wakiendelea kuitwa waasi na wahaini.
Ndugu wanahabari,
Nyaraka zinazosambazwa mitaani kwa gharama ya walipa kodi ipitiayo kwenye ruzuku ya chama ni vita ya uchaguzi ndani ya chama, ni hofu ya wahafidhina wanaowatumia watiifu wao kufanikisha lengo lao la ushindi kwa kuwachafua wenzao kwa sababu wanajua hawana ushawishi kwenye sanduku la kura, na ndio sababu ya haya yote,na hawako tayari kukubali sanduku la kura lililo huru.
Njia mbalimbali zinatumika kusambaza nyaraka hizo feki  naziita feki kwa sababu chama kiliukana waraka wa hekaya ya domokaya kwa sababu uliwarudia na kuwachafua wahafidhina wenyewe kwa hiyo wakaukana,
Huko mikoani waraka huo unasambazwa na wanachama wenye maagizo maalum kutoka kwa wahafidhina kwa malipo ya ruzuku ya chama itokonayo na kodi za wananchi,
Magazeti mbalimbali yanatumiwa kusambaza waraka huo
Lakini mtakuwa mmeona viongozi wakitoa matamko ya kuunga mkono maamuzi ya kamati kuu, huu ni usanii wa hali ya juu, maana kinachoendelea ni kwamba kuna team imetumwa kutoka makao makuu inazunguka mikoani kwa kodi za wananchi kufanya robbing za kishamba sana.
Mkakati mwingine unaofanywa na viongozi wa kihafidhina ni kupanga safu inayowatii ili wafanikishe ushindi endapo sanduku la kura litalazimishwa kuwepo,
Mwenyekiti Mbowe amekuwa akizunguka kwa siri kupanga mipango hiyo mikoani Rukwa, Kagera, Mbeya Mtwara, Tabora n.k!!
Kama vile haitoshi Mwenyekiti aliamua kuwavua uongozi baadhi ya viongozi wasio wa mlengo wake, mfano Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara kwa kisingizio cha kutofanya kazi za chama kama inavyohitajika, huku akivunja utaratibu wa kumchukulia mtu hatua kikatiba..hii ni dharau kwa katiba,
Alifika Mkoani Simiyu akafanikiwa kukusanya vijana kwa mbinu ya ajabu sana akiwapachika vyeo vya uwenyeviti wa wilaya mbalimbali za kanda ya Mash (Mara, Simiyu na Shinyanga) akafanikisha kumuweka Mbunge wa maswa mashariki Mzee Kasulumbayi kuwa mwenyekiti wa kanda.
Yote hii ni kutaka kuhalalisha chama kuwa kitega uchumi cha watu kadhaa waliojificha nyuma ya kauli mbiu ya ukombozi. Wakijua kabisa endapo Mtu asiye wa mlengo wao atafanikiwa kutwaa uongozi wao watakuwa nje ya mkondo wa kutafuna pesa za chama, hali hii husababisha kila anaetaka kuhoji matumizi ya chama kuitwa pandikizi au msaliti, lakini nithibitishe kuwa santuri hii imechuja sasa.
Ndani ya chadema ukigusa pesa utazushiwa na kuitwa pandikizi hata na mtu asiyejua misingi ya chama kwa kuelekezwa na wahafidhina,
Baada ya Zitto Kabwe kuibua hoja ya vyama vya siasa kukaguliwa, tulishuhudia mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema akimtukana na kumuita nafiki kwa sababu alikataa posho
Chama hakikutoa kauli mpaka kamati kuu inaketi lema hakuchukuliwa hatua licha ya kulilia posho ambayo ni kinyume na msimamo wa kambi ya upinzani, tena bila lema kufuta kauli zake na matusi aliyomporomoshea Mzee Shibuda kwa kuitaka posho,
Wakati ule Lema alimchafua sana Mzee Shibuda kwa sababu aliitaka posho, mpaka chama kilitoa kauli na kuahidi kumshughulikia Shibuda lakini kwa lema hakuna aliyethubutu hata kuhoji,
Licha ya posho alizolilia lakini Lema aliendelea kumtukana Kiongozi wa chama Naibu katibu mkuu wake, lakini hakuna aliyethubutu kumnyooshea kidole,
Wenye utashi walijiuliza ipo wapi tofauti ya wale vijana Mtela mwapamba, Juliana shonza na anachokifanya Lema?
Je wao walipotenda kosa la kumshambulia kiongozi walitimuliwa na mbona lema anaonekana shujaa? Utashi wa Mwenyekiti kwa jambo hili unaashiria ukabila wa Mbowe na sio ukabila wa chama, chadema haina kanuni wala misingi ya ukabila bali ni suala la utashi wa kiongozi tu
Lema ni miongoni mwa watiifu wa wahafidhina aliyetumwa kumchokoza Zitto ili Zitto amjibu wapate sababu ya kumjadili katika vikao na kumsimamisha uongozi ili akose sifa za kugombea uwenyekiti wa chama.
Waraka uliovuja kutoka kati yao walioketi nyumbani kwa mwenyekiti akiwa na wabunge wanne ulieleza kuhusu mpango huu lakini hakuna aliyeamini,
Week moja baadae yakatimia yaliyonenwa kwenye waraka wa siri juu ya mbowe kuwang’oa asiopendana nao.
Hali hii imevumiliwa sana na sasa imefikia kikomo na wapigania deomkrasia tumejitokeza hadharini kuanza mchakato wa kuuondoa utawala wa aina hii madarakani kwa kutumia nguvu ya umma,
Wengi wanauliza kwa nini tutumie mfumo nje ya ule utaratibu uliozoeleka wa kungojea uchaguzi wa chama?
Utaratibu uliopo  wa kuvumilia na kungojea mabadiliko yatokee kwa njia ya sanduku la kura ambalo mpaka sasa wameshalipaka majina ya wahafidhina huwa hauzai matunda kamwe ikizingatiwa mbinu za upangaji safu wa wahafidhina na mbinu ya upanguaji safu kwa watu wasio sukumwa bila hoja.
Mbowe Freeman ametangaza kuendelea kuwa mwenyekiti wa chama mpaka hapo atakapopatikana mtu makini wa kukiongoza chama, hii inaashiria utashi wake hasi wa kuwaamulia wanachama mtu wa kuwaongoza,lakini akihakikisha kuwa mfereji wa kunyonyea mapato unaungwa kwenye mifuko ya suruali yake ili aendelee kuwa  Procurement Officer na Chief Supplier wa Vifaa vya Chadema, aendelee kuwa Mnunuzi na Muuzaji wa kila kinachohitajika bila utaratibu wa chama kufuatwa.
Wakati wa Uchaguz 2010 ilidaiwa anasaidia Chama lakini baada ya Matokeo kaleta Invoice za Gharama za Uchaguzi na kuzoa 500Mil za Ruzuku sasa Chama kinaendeshwa kwa sadaka za kwenye Mikutano ya Hadhara, michango ya wadau na hasa Mzee Sabodo, hata juzi Sabodo ametoa million 30 kwa kusaidia ujenzi wa ofisi ya wilaya ya kigoma lakini mpaka sasa pesa hizo ziko Makao makuu ingawa aliyepokea mbele ya waandishi wa habari ni kiongozi huyo wa Wilaya.
Katiba yetu tunaiheshimu lakini imeshindwa kutusaidia, tunailinda lakini imeshindwa kutulinda.
Kama vile wabunge wa upinzani wanavyoamini katika kanuni za bunge ndivyo tunavyoiamini katiba yetu, lakini kanuni za bunge zinapokwamisha hoja za wapinzani bungeni wao huamua kutoka nje na kama sio kufanya fujo ndani ya ukumbi wa bunge, basi hutoka nje na kuamua kuandamana barabarani kulaani na kutoa kasoro za kanuni na hata kuwashambulia viongozi kwa sababu wanaamini katika nguvu ya umma
Kadhalika sisi nasi tumejifunza umuhimu wa nguvu ya umma kama wabunge wetu, na sasa kwa utashi ule ule wa wabunge wetu nje ya taratibu za kibunge nasi tunaenda nje ya utaratibu na kanuni za chama, ukombozi tunaouimba majukwaani tunahitaji tuanze ndani kwanza.
Utashi wa Mbowe ni hasi dhidi ya taasisi na hii ndio sababu anajitahidi sana kuahakikisha safu yake inakamilika kwa gharama zozote
Ukianza kufuatilia mlolongo wa watu walioitwa wasaliti au wanatumwa na ccm utagundua hoja yao ni moja tu ya matumizi ya pesa za chama hoja ambayo imemgharimu Zitto Kabwe,
Inafikia hatua wahafidhina wanasema wazi kuwa ni bora chama kishuke daraja kuliko chama kupewa mtu wa nje, mtu wa kuja, mtu wasiyemfahamu,
Leo Mzee Mtei amenukuliwa akisema ‘tumewafukuza watu tuliokuwa tukisuguana nao kwa muda mrefu sana’ hii ni dalili ya kukipaka rangi chafu chama huku wakijificha nyuma ya sauti ya ukombozi
Mantiki ya Mzee Mtei na Lema  kutoa pesa kwa vikundi vya vijana Arusha ili wafanye sherehe siku ya pili ya tukio la kuvuliwa madaraka Zitto ilikuwa ipi? Hili lilipekea watu wa mikoa mingine kuhoji kwa nini wanatengwa na chama.
Mfano:- Watu wa Mkoa Mara waliuliza tumeikosea nini chadema, kwa nini kila mtu anaetokea Mara anahujumiwa?waliuliza wakitolea mifano ya Chacha Wangwe na Mwigamba
Watu wa kigoma wao wanalikumbuka tukio la Kaburu, Kafulila, na sasa Zitto
DHANA YA UGHAIDI
Ndugu Wanahabari,
Migogoro mingi ndani ya siasa za Tanzania huambatana na mambo mengi ambayo ukweli wanaujua wasemao na wale wasemwao,
Mfano matukio ya mabomu na mutekana yameshamiri bila watu kujua ukweli wake
Hivi karibuni kuna waraka ulisambazwa mitandaoni ikieleza sakata la chadema kujiteka na kumwagia saed kubenea tindikali,
Hakuna ajuae ukweli wa jambo lile lakini pia inabidi tulishangae jeshi la polisi kwa kutofanya utafiti wa waraka ule kwa kupuuza mitandao ya kijamii,
Kunapotokea migogoro ya ndani ya vyama lolote huweza kutokea ,
Mtu anaweza kutekwa na kuuwawa na wanachama wa chama chake lakini wakajitokeza wao wenyewe na kusema kuwa chama tawala kimetumia mwanya huu kutugombanisha,
Lakini pia chama kingine chaweza kutumia fursa hiyo kuwagombanisha kweli,
Mimi leo mnaweza kusikia kesho nimeuwawa, msije mkaanza kudhani ni ccm wametumia mwanya huu kuwagombanisha chadema lakini pia mjiulize na upande wa pili kama hawawezi kunidhuru wakijua wataivisha ccm mzigo?
Kwa hili hatuna jibu.
Chadema haina sera wala dira ya ughaidi bali utashi utabaki kuwa wa mtu kama yeye.

 MSIMAMO WA WAPIGANIA DEMOKRASIA (WAASI)
Tunamuonya Zitto na Mkumbo tabia zao za kusema kuwa wanaheshimu maamuzi ya kamati kuu huku wakijua ni nini kitatokea waache mara moja kwani unyonge wa aina hii ni kuruhusu utengenezaji wa majizi na maporaji ya baadae na sisi hatuwezi kulea upuuzi wa aina hii tukingojea uchaguzi ambao kimsingi  hautaleta mabailiko tuyatarajiyo.
Na ndio sababu tumeamua kutangaza uasi huu bila kuwatarifu wala kuhitaji ushriki wao.
Tutaungojea uchaguzi tukiwa na uimara wa usimamizi wa kanuni na ufuataji wa taratibu,
Nikiwa kama BRIGEDIA wa wapigania demokrasia (waasi) natangaza rasimi mgogoro wa kiutawala kati ya wahafidhina na wapigania demokrasia
BRIGEDIA NYAKARUNGU natoa wito kwa wananchi wote walioumizwa na kulia wengine kukata tamaa wafahamu sasa tunachukua hatua kwa hawa Mahafidhina na mafisi wa mistu ya Nyamandicha,
Naamuru waliopenyezwa kukaimu nafasi za uongozi huko mikoani wajiondoe haraka kabla hatujawaondoa kwa nguvu ya umma,
KUHUSU MM2,
MM2 yupo na hakuna atakayemtaja mpaka mwenyewe atakapojitokeza siku yoyote ile kama ataona inafaa, lakini kwa heshima yake kwa vijana na chama na kuaminiwa na wahafidhina tumwache akae kati yao kwanza, lakini siku akijitokeza hamtaamini ka ndiye MM2, nadhani siku hiyo mtaamini ukweli wa haya yote.
BRIGEDIA NYAKARUNGU NATOA SIKU TANO (5) HADI TAREHE MOJA DECEMBER MWAKA HUU KUWATAKA VIONGOZI WALIONDOLEWA KUREJEA KWENYE NAFASI ZAO NA ENDAPO WATAPUUZA TUTAANZA MIKUTANO YA HADHARA KUWASIMIKA VIONGZOI WAPYA NA KILA KONA YA WATANZANIA WATAJUA JUA HILI!
Imetolea na BRIGEDIA NYAKARUNGU,
Mkuu wa kikosi cha kuisaka Demokrasia Chadema.

No comments :

Post a Comment

 
Copyright © 2013. BongoAfrica - All Rights Reserved.