skip to main
|
skip to sidebar
Rais Joyce Banda adai tena mkoa Ruvuma ni mali yake!!
Rais Joyce Banda adai tena mkoa Ruvuma na wananchi ni mali yake
RAIS wa Malawi, Joyce Banda
ametajwa kuendeleza chokochoko baina ya nchi yake na Tanzania, huku
sasa akidaiwa kutumia redio na runinga za nchini mwake kutangaza kuwa
mkoa wa Ruvuma, viongozi na wananchi wa ukanda wa Ziwa Nyasa ni mali
yake.
Aidha, amesitisha safari za meli ya mv Ilala iliyokuwa ikifanya safari
kwenye Ziwa Nyasa kusafirisha mazao na wananchi wa ukanda huo upande wa
Tanzania.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa soka
wa Mbambabay jana, Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba, alisema Rais
Banda ambaye aliibua upya mzozo wa mpaka baina ya nchi hizi mbili, kuwa
ni mkorofi kutokana na kufanya vitendo vinavyoonesha uhusiano baina ya
nchi hizi mbili kuzorota.
Komba alibainisha vitendo hivyo mbele ya Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana, akisema imefika mahali Rais Banda anapotosha ukweli
kuhusu mpaka kati ya nchi hizo mbili na kudai sehemu ya mwambao wa Ziwa
upande wa Tanzania ni yake.
Mbunge huyo alisema jimbo la Mbinga Magharibi ambalo ni Wilaya ya Nyasa,
wanasikiliza matangazo ya redio za Malawi, na anazitumia kupotosha umma
kuwa ukanda wa Ziwa Nyasa ni mali yake na wananchi wanaamini hivyo.
Rais Banda anatangaza kupitia vyombo vya habari vya nchi yake ambavyo
vinasikika vizuri katika wilaya hiyo kutokana na wilaya ya Nyasa
kutopata mawasiliano ya redio na runinga za nchini. Komba alisema
kutokana na wilaya hiyo kukosa mawasiliano ya vyombo vya habari,
wananchi wake wanakosa kusikiliza matangazo zikiwamo hotuba za viongozi
wa Taifa.
Wananchi wanakosa kusikiliza matangazo zikiwamo hotuba ya Rais Kikwete
ya kila mwezi na hotuba za viongozi wengine wa kitaifa wakiwamo Makamu
wa Rais na Waziri Mkuu.
“Kutokana na kukosekana usikivu huo, Rais Banda anatumia nafasi hiyo
kutangaza kuwa viongozi wote wa wilaya na mkoa na eneo lote ni mali
yake,” alisisitiza Komba. Aliongeza kwamba watu wote walioko
kwenye mkutano huo isipokuwa Katibu Mkuu Kinana, akiwamo Dk Asha-Rose
Migiro ambaye alizaliwa Mbambabay wote ni mali ya Rais Banda.
Mbunge huyo alisema wananchi wa eneo hili nao ni Watanzania wanaostahili
kusikia na kupata habari za nchi yao, badala ya kusikiliza nyimbo na
matangazo ya Malawi ambayo yanakuwa na ajenda zake.
Mbunge Komba alimwomba Katibu Mkuu Kinana kwenda kuhimiza kutekelezwa
haraka kwa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ya kuleta meli ili kuwa na
usafiri wa uhakika wa mali na wananchi katika eneo hilo.
Kinana alisema ahadi ya meli ya Rais, hiyo ana uhakika itatekelezwa na
kufafanua kuwa meli tatu zinatengenezwa Korea Kusini na zitakapokamilika
ya Ziwa Nyasa itapelekwa kutoa huduma.
Alisema baada ya Banda kuondoa meli hiyo wananchi wa Mbambabay wanatumia
boti dogo kusafirisha abiria na mizigo, hali ambayo inatia shaka.
Kinana alisema amesikia kilio cha Mbunge Komba, kwamba ahadi ya Kikwete
itatekelezwa ili kuwapa wananchi usafiri wa meli, ingawa itatumia muda
kutokana na kuhitaji muda mwingi kubuni na kutengeneza.
CHANZO: HABARI LEO
No comments :
Post a Comment