SIASA ZA LEO NA FALSAFA YA ‘UHITAJI WA ARIKA’
Ninapotazama mihemko ya ushabiki wa siasa kwa vijana
kushabikia siasa au kuwashabikia wanasiasa kipindi hiki, nakumbuka falsafa ya
''UHITAJI WA RIKA'' niliyoibuni mwaka 2012 na kuiweka kwenye kurasa za KITABU
CHANGU kiitwacho ''UTASHI NI MTU''......falsafa inasema..
“Kuna wakati rika fulani huibuka na mihemko
inayofanana kwa muda wa wakati wao, rika hili hushabikia au huiga na kufanya
kitu/jambo fulani linalofanana, lakini rika la wakati wao likipita kila kitu
hupita kisha huja rika jipya na mihemko yao mipya juu ya kitu kipya.
Karibia 60% ya rika lao hushabikia kitu cha aina
moja, lakini hufikia wakati rika hili nalo hupita na huja rika jipya lenye
mihemko ya uhitaji wake mwingine.
Ukomo wa rika hutokea pale tabia zenye kufanana miongoni mwa rika
hilo huanza kuhama, wakati ambao kila mmoja hufuata njia yake kimawazo na
kifikra, hakuna ukomo wa umri katika tabia za uhitaji wa rika”
Naomba nijadili falsafa yangu kwa mifano hai,
nitatumia mfano wa muziki wa kizazi kipya maarufu kwama bongo fleva ili niweke
ufanano wa kiushabiki ulioibuka miaka ya 1990 na ikakoma kati ya mwaka
2005/2006.
Tukumbuke miaka ya 1998 -2006 enzi la Kuibuka kwa
makundi ya Muziki wa kizazi kipya hapa Tanzania Makundi kama vile:-
KWANZA UNIT, SAREHE JABIR(Solo Artist na mwanzilishi
wa rap ya Kiswahili kwa wenye kumbukumbu nzuri watakumbuka mashairi yaliyombwa
‘naruka kama ninja, natua kama ndege’),
TWO PROUD (kwa sasa anajulikana kama Sugu aliyeufanya muziki huu kupiga hatua
ya kuanza kuuzwa), WATEULE,WABABE CRAK, GORILA KILLERS, HBC(Nigga Jay,Terry
Fanani na Bigie Willy) , kundi la DIPLOMAT (Saigoni na wenzake), BALOZI DOLA
SOUL, JAMES DANDU (MTOTO WA DANDU) huyu ndiye mwasisi wa tuzo la Kill Music
Award wakati huo zikiitwa Tanzania Music Award n.k,
Nimetaja makundi na wasanii wa muda mrefu kidogo
waliokuwa na dhamira kubwa ya wazi ya kuona Muziki wa kizazi kipya Tanzania
unakuwa imara na wenye tija,Wasanii hawa wengine ni marehemu hivi sasa na
wengine bado wapo hai na wengine wapo kwenye muziki lakini wengine wamekaa
kando baada ya kufeli kwa jitihada zao za kuupigania mfumo wa kimuziki.
Wasanii hawa hawakupigania mafanikio ya mifuko yao
pekee bali walipigania mfumo wa kimuziki uwe imara na wenye tija kuanzia kwao
mpaka urithiwe na kizazi kitakachofuata baadae.
Baadae kizazi kile cha muziki uliokuwa wa dhamira ya
kutengenza mfumo wa muziki kilipita kikaibuka kizazi cha rika la wasanii wa
upepo wanaoenda na matukio walioamini si muda wa kuimba matatizo ya jamii wala
kupigania kutengeza au kubadilisha mfumo wa soko la muziki, bali ni muda wa
kuburudika tu na watu wasahau shida zao kwa muda, walipigania nyimbo zao
kupigwa redioni wakiamini ndio mafanikio na wakipata mialiko ya kutumbuiza na
kulipwa pesa ni mafanikio makubwa kwao.
Wasanii hawa waliamini kuzalisha albamu na kuuza ni
sehemu ya mafaniko, waliamini pia kujulikana sana kila kona ya nchi ni
mafanikio tosha.
Hakuna aliyekumbuka kusimamia misingi iliyoasisiwa
na waasisi wa sanaa hii iliyopendwa sana kwenye jamii, pengine waliamini hatua
waliyoifikia ndiyo mafanikio na hakuna mafanikio zaidi ya hayo.
Walikabidhi akili zao mikononi mwa waliowaita
mameneja, wasambazaji na watangazaji wa redio kadhaa, wakaagizwa kutunga nyimbo
kwa namna wakubwa wao walivyotaka, wakaagizwa hata kiwango cha kulipwa na
wakaagizwa kutoshirikiana na baadhi ya wasanii walikuwa kundi lisilo na
mapatano na wakubwa zao.
Miaka hii
tunakumbuka kulikuwa na mihemko ya vijana wakiibuka na kufanya muziki wa kizazi
kipya.
Kila mkoa, kila wilaya, kila kata, kijiji na pengine
karibia kila kaya usingekosa mtu anaejiita msanii, anaesuka nywele bila kujali
jinsia yake, anaevaa jeans kwa mtindo wa KK, anaetembea amekunja bega moja na
hata waliovuta bangi sio kwa sababu ya asili yao bali kwa sababu ya mihemko ya
kudhania kuwa kuwa msanii lazima uvute bangi kwa ufupi muziki huu ulipendwa kwa
asilimia kubwa ya jamii.
Bongo fleva iliwatoa wengi kimaisha, kiumaarufu,
hata kimaslahi mengine waliyoyajua wenyewe, mradi tu iliwatoa.
Wakati ule kila msanii aliyetoa single redioni
tulitarajia na baadae tukashuhudia tamasha kubwa la uzinduzi wa album yake, kwa
wengi kipindi kile walipoingiza sokoni album waliuza sana, kipindi hicho
walisambaziwa na kampuni moja tu ya wahindi (GMC) iliyoko kariakoo inamilikiwa
na MMAMU,
Waliuza sana tapes (kanda) na walitoka kwa kweli, na
wengi wao mie nilishiriki harakati zao kimuziki ikiwa ni pamoja na kutengeza
beats zao katika studio kadhaa hapo bongo miaka ya 2003 -2005 na wengine
kutumia mashairi yangu niliyowapa kwa hiyo nawafahamu na ninaujua muziki wa
bongo vilivyo.
Lakini kizazi cha rika lile kilipoondoka hatukuona
tena kitu kinaitwa uzinduzi wa album pale Diamond jubilee wala club billcans,
wala tour za mikoani za kutangaza album hazipo tena, mbaya zaidi hata tapes
hazikuzalishwa tena ukiachilia kutonunuliwa kwake,
Utakumbuka wakati ule ferouz na kundi lake la
Dangers of Zone Nundaz (Daz Nundaz), Mr
Nice, Jay Moe, Mr Blue, Dully Sykes n.k walivyokuwa wakifanya vizuri kwenye
media na mitaani kwenye matamasha yao.
Walitamba na kuufanya muziki kwa style yao wakisahau
mifumo ya soko imekaa kihamasa tu na sio ya kudumu, wakasahau siku moja zamu
yao ya hamasa itapita bila kujali uwezo wao mzuri wa kimuziki, wakaacha upepo
wa hamasa ya muziki iwaendeshe mpaka walipofika ukomo wao.
Leo hii wapo wanajitahidi kurudi lakini wananchi
waliopo sio wale wa uhitaji wa rika lao, wanaimba ujumbe safi na mkao wa
kimuziki lakini hakuna anaepokea muziki wao, ni kwa sababu wao waliruhusu
muziki wa hamasa na kusahau hamsa yao itapita, kosa walilolifanya ni kushahu
kusimama kwenye mabadiliko ya kimfumo wa muziki na soko lake, wakaruhusu
watangazaji kuwa mabosi wao na matajiri kadhaa kuwashika na kuwaamulia watakalo
wao, ndio ikawa mwisho wa vita ya kupinga mfumo wa hovyo waliyoianzisha waasisi
wa muziki wa kizazi kipya.
Hii ni dhahiri kuwa wafanyabiashara walisoma alama
za nyakati kuwa rika lao la biashara halipo tena, hata Mr Nice aliwahi kukiri
kuwa nyimbo za TAKEU hazina soko tena kwa sababu waliokuwa wakizipenda ni
watoto wa enzi zile na sasa wameshakuwa watu wazima na haoni umuhimu wa kuimba
tena nyimbo hizo kwani hazina soko.
Kilichobaki kwenye huu mziki ni wasanii tu lakini
sio wale mashabiki wala wateja wa awali, hivi sasa wasanii kwa kujua kuwa
hakuna wateja nao hawana mpango wa kuuza kazi zao bali wanauza show tu, ''nipe pesa nipande jukwaani niimbe, acha
watu wakopi nyimbo zangu kwenye flash disc zao wasikilize popote ili wawe
oriented na nyimbo zangu nipate show''.nukuu toka kwa msanii maarufu sana
hapa Tanzania asiye na mpango wa kutoa album
Katika siasa za sasa za dunia yote wala sio Tanzania
tu, mihemko hii ya uhitaji wa rika imetia fora.
Napenda kuwaomba vijana watambue kuwa kwenye hii
mihemko ya uhitaji wa rika ni mizuri endapo tutaitumia vizuri, tukadumu nayo
kwa ari tuliyonayo kwa mwelekeo wenye dira na ndoto sahihi kwa Taifa letu.
Waasisi wa Mataifa mengi ya Afrika walihakikisha
wanatengeneza mifumo ya utawala bora, wengi wakifanikiwa na wengine
walikwamwishwa kama walivyokwamishwa waasisi wa muziki wa kizazi kipya.
Mfano wa nchi ambazo mifumo ya kiutawala lifanikiwa
kuwekwa na kusimamiwa ni pamoja Tanzania, Mwalimu Nyerere alihakikisha
anatuwekea mifumo yenye miiko na inayoelekeza maadili.
Wengi wa waliokuwa kwenye baraza lake la mawaziri na
mfumo wa uongozi wake wanajua namna ilivyokuwa hatari kwa mtumishi wa umma
kutajwa kuhusika na rushwa au ufujaji wa mali za umma, hiyo haikuwa ukali wa
mwalimu bali mfumo ulipata msimamizi imara asiyetia shaka.
Baada ya mwalimu kung’atuka ndipo mambo mengi
yalianza kwenda kombo, kama ambavyo kizazi cha akina James Dandu kilipopita
kikaja kizazi cha akina Feruz na Mr Nice na sanaa za hamasa wakasahau kuwa
mafanikio yao ya kuuza sana santuri zao bila kuimarisha mfumo wa soko ni hasara
kwa wasanii wa baadae.
Kadhalika alipokuja mrithi wa serikali ya Mwalimu
nae alivaa uhusika wa hawa akina feruz, akajikuta akiyumba na kuzungukwa na
wakubwa wenye tama za ubwanyenye wa kutumia nafasi zao katika kufuja mali za
Umma bila kujali kizazi cha baadae kitaumia.
Hapa ndipo siasa za hamasa za nani mbwatukaji jukwaani,
nani mtoa rushwa mzuri ili achaguliwe, nani mwenye maneno matamu jukwaani n.k zilipoibuka ni kwa sababu ya kuacha mbio
za kuimarisha mfumo wa maadili ya Utaifa wetu na kuanza kuendeshwa na hamasa na
siasa za upepo.
Hapa tukashuhudia vita kati ya mwanasiasa mmoja na
mwingine, vita baina ya kundi moja na jingine, mashabiki wa upande wa mwasiasa
na mwingine bila kujali kesho ya kizazi kijacho kama walivyoingia mkenge akina
Profesa Jay (Nigga Jay) kwa kuacha alichokuwa akipigania zamani na kuzama kwenye
mbio za hamasa, kadhalika viongozi wetu wakaacha mbio za kuweka na kuajadili
issues na wakaanza kutafuta maneno yanayoweza kuwavutia watu wapige makofi tu.
Wakati ule wa Bongo sanaa, niliwahi kushudia
mashindano ya mfalme wa rymes, wakati Afande Sele the King (moja ya wasanii
wanaotumia akili sana kuandika mashairi na kuufanya muziki wao kutokushaka
thamani) wa MOROGORO aliibuka kidedea.
Wakati ule kila kijana alikua akishabikia msanii
anaempenda, ilifikia hatua wasanii wakawa na ugomvi baina yao na kuwafanya
mashabiki wawe na ugomvi wa kiushabiki kama wale wanaowashabikia.
Kadhalika kwenye siasa hivi sasa hakuna tofauti na
wakati ule vijana wanaodhani siasa ni burudani kama ilivyokuwa sanaa.
Siasa ni mfumo wa kutengenza mbele ya Taifa,
tutofautiane kifikra, kimtazamo na kiitikadi lakini tusitofautiane kwenye lengo
kuu (kutengenza Taifa imara).
''Uwe na malengo yako, yenye utofauti na ya
mwingine, lakini yote yalenge kutimiza lengo kuu – Nukuu yangu toka kwenye
kitabu change cha “UTASHI NI MTU’’.
Wapo wasiojua tofauti ya vyama vya siasa na Taifa au
Serikali, hawa wapo tayari hata kupinga Jakaya Kikwete kuitwa Rais, wapo pia
wanaodhani tofauti ya itikadi ndio tofauti ya malengo makuu ya siasa za nchi
(wanahitaji shule)
No comments :
Post a Comment