Saturday, November 30, 2013

MWENYEKITI WA CHADEMA MKOA AJIUZULU...!!

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI YA NDUGU ALLY O. CHITANDA

NDG: WANA HABARI:
Kwanza kabisa ninawashukuru kwa kuitika wito wangu.

Jina langu naitwa ALLY OMARY CHITANDA, nimejiunga CHADEMA mwaka 2003 nikitokea NCCR –MAGEUZI.

Nyadhifa nilizowahi kuzishika na kukitumikia Chama ni:-

Kuanzia mwaka 2004- Mjumbe wa Baraza kuu Taifa nikiwakilisha vijana Bara niliendelea kuaminiwa na Chama na kupewa kazi nyingine za kukitumikia Chama, nimewahi kuwa Afisa wa Vijana Makao Makuu, Afisa wa sheria na Haki za binadamu Makao Makuu, Katibu wa Kamati ya muda ya Baraza la Vijana Taifa (BAVICHA) kwa sasa ni Mjumbe wa Mkutano Taifa nawakilisha Nachingwea, Mwenyekiti wa Mkoa wa Lindi tangu tarehe 26/05/2013.Pia ni Afisa Mwandamizi Ofisi ya Katibu Mkuu Makao makuu Dsm.

vile vile kwa kipindi kirefu sasa nimekuwa nikifanya shuhuli ya uandishi wa kumbukumbu za sekretarieti ya chama kama KATIBU WA SEKRETARIETI YA KAMATI KUU.
Hivyo sasa, pamoja na mambo mengine yapo masuala nyeti na muhimu ninayoyafahamu na ikibidi kuwaarifu watanzania kwa njia mbali mbali pindi itakaponihitaji kufanya hivyo.

Ndugu zangu wanahabari, nimewaita ili kupitia nyinyi niwaambie Watanzania wenzaqngu juu ya hali ya kisiasa ilivyo hasa ndani ya Chama chetu. Itakumbukwa kuwa tarehe 20-21/11/2013 Kamati kuu ya Chama ilikaa pamoja na mambo mengine ilifanya maazimio ya kuwavua nafasi za Uongozi ndani ya Chama alikuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara Mhe. ZITTO KABWE na Mjumbe wa Kamati kuu wa kuchaguliwa Mhe. Dr. FITILA MKUMBO, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kwa sababu:-

(a) Mhe. ZITTO KABWE (Mb) alishiriki kusaidia Wabunge watatu wa CCM kupita bila kupingwa kenye Majimbo yao ya Uchaguzi 2010.

(b) Kuandaa mkakati waliouita mabadiliko ya Chama 2013. Mkakati uliolenga kumuwezesha Mhe. Zitto kushinda nafasi ya Uenyekiti wa Chama Taifa endapo angekubali kugombea.

(c) Mhe. Zitto alishindwa kutimiza majukumu yake ndani ya Chama kwa kutoshiriki pamoja na Viongozi wenzake kwenye matukio makubwa yaliyokikumba Chama kama:-
(i) Maandamano ya Arusha.
(ii) Operesheni zilzofanyika Morogoro na Iringa nk.

MAAMUZI MENGINE YA UBORESHAJI WA MAKAO:
Ni kweli kuwa pamoja na mambo mengine Baraza kuu la Chama iliridhia pendekezo lililetwa kwake na Kamati Kuu kuhusu jambo hili.Na katika utekelezaji wake Kamati Kuu ya juzi iliridhia kuwa, uteuzi wa Wakurugenzi watano ambao ni:-
1. Mkurugenzi wa Oganaizesheni Mhe. Singo Kigaila Benson.
2. Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano ya ndani Mhe. John Mnyika (Mb).
3. Mkurugenzi wa Fedha na uwekezaji Mhe. Anthony Komu.
4. Mkurugenzi wa Bunge na Halmashuri Mhe. John Mrema.
5. Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama Mhe. Wilfred Lwakatale.

Uteuzi huu hauonyeshi sura ya Kitaifa Wakurugenzi wote watano ni Wakristo kanakwamba CHADEMA hakuna Waislamu wenye uwezo wa kushika nafasi hizo.

Lakini pia hauzingatii mgawanyo wa kijamii kwa kuwa kati ya kurugenzi hizo sita wakurugenzi wanne kati yao wanatokea mkoa mmoja wa kilimanjaro

Na uteuzi huu unakwenda sambamba na kuboresha maslahi yao kwa kuongeza posho, -kutoka Tshs. 800,000/= za awali na sasa itakuwa ni kuanzia Tshs. 1,500,000-2,500,000/= kwa Mkurugenzi na kutoka Tshs. 6,800,000/= kwa Afisa Mwandamizi na sasa ni Tshs.1,000,000-1,500,000/=.

Pamoja na kwamba uboreshaji uliridhiwa, lakini katika mpango ulioridhiwa na Baraza kuu ni pamoja na kulipa Posho kwa Makatibu wa Wilaya na Mikoa. Hawa ndio watendaji muhimu katika Ujenzi na Uhai wa Taasisi hii lakini, hawakuangaliwa wala kuguswa badala yake wanatakiwa kujitolea tu kwa hali na mali.

Mimi kama nilivyotangulia kusema hapo awali, kuwa niko kwa kwa miaka 10 sasa na nimeshiriki kwa kiasi kikubwa katika Ujenzi wa Chama hiki.Sioni sababu ya kutoharakisha kulipa posho ya Mkatibu wa Wilya na Mikoa pamoja na watendaji wengine na badala yake tunaharakisha kujilipa posho nono sisi watendaji wa Makao Makuu, wakati hawa wa ngazi za chini wanamaeneo makubwa ya Kiutendaji na wanafanya kazi katika mazingira magumu kwa kujitolea hata Ofisi zao wanajitolea wenyewe.

MAAMUZI YA KAMATI KUU
Ningependa kuwaambia wanachadema na watanzania kwa ujumla, maamuzi haya ya kamati kuu ya kuwavua uongozi zitto kabwe na dkt mkumbo ni maamuzi ya kijuha na yanayowafanya watanzania sasa waangalie mara mbili mbili kama hawa watu wapo makini na huo ukombozi wanaousema.

Tumekuwa tukiweka mikakati mbali mbali ya ushindi ili chama kishinde, kwa mfano, kabla hata ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa arumeru mashariki, wakati tu ilipobainika anaugua, chama kiliandaa mkakati wa kushinda ubunge wa jimbo hilo na uchaguzi uliporudiwa mkakati ule ulitumika na kushinda.

Nikiwa mtendaji wa ofisi ya katibu mkuu, nimeshiriki pamoja na zitto kabwe na dkt Slaa kupanga mikakati mbali mbali mizuri na mibaya kwa nchi, lakini hatukuwahi kuitwa wasaliti, wahaini wala sina lolote baya. Ni fedheha leo mimi kuwa sehemu ya watu wanaomuita zitto kabwe ni msaliti. Siwezi kuendelea na ujinga huu na sipo tayari tena.

Si dhambi kumuhukumu mtu kwa kuwa anapanga mipango ya kukushinda kwenye uchaguzi, dawa ya mpinzani wako ni kumkabili.

Naomba nikiri kwamba nikiwa katibu wa sekretarieti tumekuwa tukilazimishwa mara kadhaa kuwashawishi wajumbe wengi kutowaunga mkono watu wenye misimamo thabiti ndani ya chama na badala yake tumekuwa tukitumia rasilimali za chama kuwajenga wajumbe ndio.

Kwa mfano hivi sasa tunapozungumza, wakati katibu mkuu wa chama anasema mjadala wa zitto kabwe umefungwa rasmi, amewaagiza wakurugenzi wa chama kuzunguza nchi nzima kusambaza waraka waliouandaa ukimchafua zitto. Hii si sawa hata kidogo, si vema kutumia rasilimali za chama kuwanufaisha watu binafsi kutimiza matakwa yao ya kisiasa.

Nafsi yangu haipo tayari kuendelea kuwa sehemu ya upotoshaji dhidi ya watanzania wenzangu.

Nafsi yangu inanikataza kabisa kuendelea kufumbia macho maovu yanayoendelezwa na chama changu.

Nafsi yangu imechoka kuendelea kushuhudia ubaguzi wa kidini na kikabila unaofanywa wazi wazi na viongozi wa chama changu.

Nafsi yangu imekataa sasa, haipo tayari tena kuwa kuwadi wa kuwahadaa Watanzania kuyafikia matarajio tunayowapa ambayo kamwe hayafikiki.

Kwa kuwa siamini kwamba kuvuliwa nyadhifa kwa zitto kabwe na dkt kitila mkumbo ni kwa sababu ya waraka wa ushindi, bali ninaamini kuvuliwa kwao ni kutokana na hofu ya uchaguzi, ubaguzi wa kikabila na kikanda.

Hivyo basi, nikiwa na akili timamu kabisa, leo tarehe 30.11.2013 nimeamua kujivua nyadhifa zangu zote nilizokuwa nazo ndani ya chama.

Sioni tena sababu ya kuendelea kuwa MwanaCHADEMA, sioni tena sababu ya kuwa mwenyekiti wa CHADEMA MKOA WA LINDI, sioni tena sababu ya kuwa KATIBU WA SEKRETARIETI YA KAMATI KUU.

Kwa kuwa vipaumbele vya chadema ni kukijenga chama mikoa ya kaskazini. Basi sisi wananchi wa mkoa wa lindi tunawatakia kila la heri, na kwamba waendelee kukijenga chama chao huko huko waliko.

Nashukuru wote ambao nilifanya nao kazi pamoja katika kutekeleza majukumu yangu.

Ahsante Sana

A.O. CHITANDA

0753418510

MWENYEKITI CHADEMA MKOA LINDI
MJUMBE BARAZA KUU TAIFA
KATIBU OFISI YA KATIBU MKUU- SEKRETARIETI

1 comment :

 
Copyright © 2013. BongoAfrica - All Rights Reserved.