SIRI
ya mgogoro kati ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Bodi
ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) iliyovunjwa hivi karibuni imewekwa
hadharani, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Waraka
ulionaswa na gazeti hili ulioandaliwa na mmoja wa waliokuwa wajumbe wa
bodi hiyo, umeainisha kuwa hatua ya Waziri Mwakyembe kuivunja bodi hiyo
kulilenga kumlinda Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Madeni
Kipande, ambaye bodi hiyo ilipanga kumng'oa madarakani.
Kwa
mujibu wa waraka huo unaodaiwa kuandaliwa na aliyekuwa mjumbe wa Bodi
ya TPA, John Ulanga, uliovuja katika mtandao wa Jamiiforums.com hivi
karibuni, umebainisha kwamba sababu kubwa ya Dk. Mwakyembe kuvunja bodi
hiyo ilikuwa kumuokoa Kipande ambaye bodi ilishamuona hafai kuongoza
mamlaka hiyo na kutaka kumuokoa.
Katika
waraka huo mrefu, Ulanga ameanisha sababu na uwezo wa kisheria wa bodi
kumuondoa Kipande, waraka ambao haukujadiliwa kutokana na Dk. Mwakyembe
kuivunja bodi siku moja kabla ya kuwasilishwa kwake.
Hata
hivyo, Ulanga ambaye ni mwanasheria anayeongoza taasisi inayoheshimika
ndani na nje ya nchi ya Foundation for Civil Society, anaelezwa na watu
walio karibu naye kwamba amekerwa kuvuja kwa waraka huo, hasa baada ya
yeye kuwa mmoja wa watu waliokuwa wakituhumiwa na Kipande kuwa ni
wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutokana na
msimamo wake.
Mmoja
wa wajumbe wa bodi ya sasa ameliambia gazeti hili kwamba hata wao
hawana uhuru wala amani kwa kuona kilichozipata bodi zote mbili
zilizopita na ambazo zote anaamini ziliundwa na watu makini lakini
zikashindwa kufanya kazi chini ya Waziri Mwakyembe.
Katika
waraka huo, imeelezwa kwamba Kipande ameonyesha kiburi na dharau kwa
bodi kwa kushindwa kufuata maagizo (mapendekezo) ya bodi na badala yake
amekuwa hata akiwadhalilisha wajumbe wa bodi kama anavyofanya kwa baadhi
ya wasaidizi wake.
Tuhuma
nyingine zilizoanishwa dhidi ya Kipande ni pamoja na; jinsi
alivyoendesha uajiri wa viongozi wa juu kinyume cha maagizo ya bodi;
ubaguzi dhidi ya wafanyakazi, watu wa makabila tofauti; chuki na Wana
CHADEMA; kuingia kwenye mikataba bila kufuata taratibu hasa kwenye suala
la e-CTN; kuchelewesha utekelezaji wa "Big Results Now" na kumdanganya
waziri kuhusu mapato ya TPA.
Kwa
kutumia takwimu za Kipande ambaye hakuwa akiwashirikisha wataalamu
wake, Waziri Mwakyemba amekuwa akitangaza kwamba Bandari ya Dar es
Salaam imeongeza makusanyo yake kutoka sh bilioni 28 hadi sh bilioni 50
huku akijua kuwa si sahihi.
Mamlaka ya Bandari imekuwa ikizingirwa na tuhuma luluki huku wananchi wakiendelea kuaminishwa kwamba hali ni shwari.
Hali
hiyo imeathiri kwa kiasi kikubwa uchumi, kutokana na bandari kuwa lango
kuu la uchumi kwa Tanzania na nchi jirani zisizo na bandari.
-CHANZO TANZANIA DAIMA
No comments :
Post a Comment