Wednesday, December 18, 2013

Gazeti la MwanaHabari Makala ya fikra mpya tarehe 16 december 2013

DHANA YA UMRI WA URAIS.

Na Nyakarungu Grayson,
Salaam wasomaji wote wa ukurasa wangu,

Kwanza nawapa pole kwa mihangaiko ya kutimiza majukumu yenu  katika juma zima,
Majuma kadhaa yaliyopita nilijikita katika kujadili mihemko ya kisiasa inayoendelea Tanzania makala ilibeba kichwa kilichosomeka ‘Siasa za leo na Falsafa za uhitaji wa Rika’ makala yake sio tu kwamba yamewapa watu elimu juu ya aina mbaya ya siasa tunaifanya hapa nchini bali yamefanikisha mabadiliko makubwa ya watu waliotafakari vyema ujumbe na maudhui yake.

Leo naomba kuzungumzia dhana ya umri katika uongozi, kuna uongozi wa aina nyingi, pia uongozi una madaraja mbalimbali kutegemeana na aina ya Taasisi au Taifa lilivyojipangia madaraja yake,

Wapo viongozi wa vijiji, viongozi wa kata, viongozi wa wilaya, viongozi wa mikoa , viongozi wa kanda na  viongozi  wa Nchi nzima,
Leo katika makala hii nitajikita kuongelea daraja la juu kabisa la uongozi wa Nchi,
Nitatumia daraja la Urais ambalo ni cheo kikubwa na cha mwisho kwenda juu  katika nchi nyingi zinazofuata mfumo wa kimagharibi kama Marekani, Tanzania, Kenya, Afrika ya Kusini na nchi nyingine nyingi.

Katika nchi hizi zote kiongozi mkuu wa nchi na amiri jeshi mkuu wake huitwa Rais, lakini pia kwa nchi nyingine kama Ujerumani, Uingereza na nchi nyingine zina mifumo na Majina ya kuwaita viongozi wao wa juu kabisa ambao hawaitwi Rais wa nchi bali huitwa jina jingine kwa kadri ya utaratibu wao wa kihistoria katika chimbuko lao na mapokeo yao,

Zipo nchi hazina kiongozi anaeitwa rais bali anaitwa Waziri Mkuu, Mfalme au Malkia,
Huu inatoakana na matokeo wa kihistoria za nchi zao tu na namna walivyopokea au walivyokataa mapokeo ya kigeni,

Lakini tofauti ya majina ya rais wa Marekani na Waziri mkuu wa Uingereza hazileti tofauti ya vyeo vyao kiutendaji katika mataifa yao,
Mamlaka ya rais wa Marekani hayana tofauti na mamlaka ya kiutendaji ya juu kabisa ya Waziri Mkuu wa Uingereza.

Nafasi ya juu ya kiutawala ya nchi ina sifa zake, ina upekee wa aina yake, ni nafasi ya mwisho kabisa kwenda juu katika Taifa.
Urais wa nchi ni daraja linalohitaji kiongozi wake awe mwenye umakini mkubwa na uwezo wake uwe usio tia shaka, aina yake ya maamuzi iwe ya kupigiwa mfano na utukuzi wake uwe unasanifu uhalisia wake.

Rais wa Nchi ni Mtu anaetakiwa kuwa mkomavu wa kiutendaji, awe mwenye historia nzuri ya kiutendaji mwenye historia ya uadilifu na mwenye nguvu za kimamlaka,
Rais wa nchi awe Mtu mwenye heshima mbele ya jamii yake na jamii isiyo yake.
Sizungumzii mgombea wa Urais wala siongelei Mtu mwenye uwezo wa kushinda bali natoa wasifu wa jumla wa Mtu anaetakiwa kuwa Rais.

Umri wa Mgombea Urais ndio unaweza kutoa majibu ya maswali au wasifu nilioueleza hapo juu,
Kwa hii sifa ya umri wa mgombea mtu mwenye umri mkubwa ndiye anapata nafasi kubwa ya kutambulika kwa sifa hizo hapo juu,

Mfano, hatuwezi  kufahamu uwezo wa kibusara za kiuongozi kijana mwenye miaka 35 ambaye hajawahi kuwa kiongozi katika nafasi za juu za nchi, pia ni vigumu kufahamu uwezo wa kiutendaji wa kijana mwenye umri wa miaka 35 ambaye ndio kwanza amehitimu shahada yake ya kwanza chuo kikuu.

Pia ni vigumu kufahamu  maamuzi ya kiheshima anayoweza kuyafanya kwa ndani au nje ya nchi kwa kijana wa umri huo wa miaka 35 asiye na historia ya matendo hayo au inayofanana na hayo,

Hii yote haina maana kuwa vijana hawafai  au hawana uwezo wa kuongoza, bali kinachomata ni historia inayoweza kutumika kuwaaminisha watu kama ushuhuda wa uwezo wa kijana anaeomba kuongoza Taifa.

Kama sifa hizo hapo juu zikipatikana kwa kijana, basi kijana anaweza kusimama  kwa nguvu ya andiko la Mtume Paulo la kuwa anawaandikia vijana kwa kuwa wanazo nguvu, ikiwa kijana amebahatika kuonyesha uwezo wake katika nafasi kadhaa alizopewa licha ya umri wake kuwa mdogo, basi anaweza kufaa zaidi kuliko kuamini katika vichwa vyenye mvi au vipara pekee.

Umri unawanyima vijana sifa ya wao kuwa na ushuhuda wa historia ya uongozi, hii ndio sababu inayowafanya vijana wengi kukwama hata kwenye usaili wa kazi katika mashirika au makampuni mbalimbali duniani kote,

Kwa sababu mwajiri anahitaji mtendaji wa kazi atakeiwezesha taasisi yake kuimarika na kuhitmisha mafanikio yaliyotarajiwa, ndio sababu waajiri wengi hutaka kujilidhisha pasi na shaka juu ya uwezo wa muomba ajira kwa kuhoji uzoefu wake kwanza.

Kadhalika kwenye hili watu wenye uzoefu mkubwa hufanikiwa kuajiriwa kwa kuaminiwa kuwa uzoefu wao utarahisisha kazi, wakati huo huo watu wasio na uzoefu huachwa sio kwa sababu ya taaluma yao kutokidhi vigezo bali ni kwa wao kushindwa kuwa na ushahidi wa uwezo wao licha ya kufaulu vyema masomo ya nadharia.
Ukitazama watu wanaomba kuwa viongozi wa Taifa lolote Duniani utagundua historia zao zinavyowabeba au zinavyowaangusha,

Hii kwa watu wenye umri mkubwa ni fursa kwao kuyatumia matendo yao ya nyuma kujitetea na kujiuza mbele za jamii ili wapate kibali.
Kwa kijana asiye na historia ya uongozi  huwa ni kazi ngumu sana hata kufukiriwa licha ya uwezo wake wa akili na ubunifu ambao hajapata nafasi ya kuuonyesha,

Hii ndio sababu kijana anapotangaza nia ya kutaka kugombea nafasi hiyo kubwa ya nchi watu wengi huanza kuguna si kwa kigezo cha uwezo wake,bali ni kwa sababu za mashaka juu ya uwezo wake wasio na ushahidi wake.
Hii yote ni kwa sababu wananchi hukosa uhakika wa uwezo wa kiuongozi wa kijana anaewaomba ridhaa

Sifa hizi kwa wenye vipara na mvi ni  rahisi kujua kama wanazo au hawana, kwa sababu wamebahatika kuishi kwingi na kama ni mengi wameyaona , kati yao wapo walioweza kuijenga historia yao vyema kwa umadhubuti wa utendaji kazi, lakini kati yao wapo waliofanikiwa kuonyesha uhafifu wa uwezo wao kiutendaji.

Ikiwa mtu mwenye miaka 50+  atajitokeza kuomba kuwa Rais ni rahisi sana watu kumuhukumu kutokana na historia yake ya uongozi huko nyuma,
Mtu mwenye sifa za urais huonekana tangu anapopata nafasi ya kuongoza ngazi ya chini kabisa, hekima zake kwenye maamuzi, uwezo wake kiutendaji, ubunifu wake na usimamiaji wake kwa walio chini yake zote hizi huonekana kwake zikiwa na sura moja wapo kati ya sura hasi na sura chanya,

 Kwa sura hasi huonesha hana uwezo wa nafasi hiyo na endapo atapewa nafasi ya juu ataharibu zaidi,
Kwa  sura chanya huonesha uwezo wake mzuri umeonekana na endapo atapewa nafasi ya juu zaidi atafanikisha mipango ya taasisi au Taifa vyema.


Umri mkubwa wa mgombea huwaondoa watu wasiwasi kwa sababu wananchi hujiridhisha pasi na shaka kuwa anafaa au hafai kutokana na historia yake ya nyuma katika uongozi.
Kwa kijana mdogo licha ya uwezo wake kwa wakati huo, bado wananchi hujiuliza juu ya historia ya uwezo wake wa kiuongozi na hii imekuwa changamoto sana kwa vijana barani Afrika,
Hata Andy Rojaelna Rais wa Madagascar aliposhinda kuwa Rais wa Nchi hiyo akiwa na umri mdogo marais wengi barani Afrika hawakufurahi na uhusiano kati yao na yeye uliyumba.

Sio kila mzee anafaa kuwa Rais  na sio kila kijana hafai kuwa Rais, bali uwezo wao ndio unaoweza kuwatabainisha kwa jamii juu ya sifa zao za nafasi hiyo ya juu kabisa katika taifa.

Kwa sababu hii wazee wanapata fursa kubwa ya kuonekana kufaa kwa sababu ya historia zao  za utendaji,
Ikifika wakati wa kuomba ridhaa majukwaani au ukumbini utagundua urahisi wa mgombea mzee kujinadi na utagundua ugumu wa kijana kujinadi kwa mfano hii hapa chini;-

Wakati kijana akihangaika kueleza anavyojua kukokotoa mahesabu lakini mzee yeye huwakumbusha watu alivyotetea bei ya pembejeo kushuka na masoko ya tumbaku wakati akiwa waziri wa wizara husika,
Wakati kijana akijieleza alivyofaulu vizuri soma la mahusiano ya kimataifa, mzee yeye huwakumbusha wananchi alivyomleta Rais wa Marekani kutembelea kijiji chao na kupanda miradi ya maji.

Mzee akigundua tofauti yake na kijana kwa upande wa historia huamua kuwashawishi watu wasimpe nchi mtu anaetaka kwenda kujifunzia uongozi ikulu, wakati huo kijana hujikita katika kuwashawishi watu wasipe nchi mtu aliyezeeka hana jipya
Ikifikia hapo kijana hukosa sifa kwa sababu  ya historia ya kiutendaji,

Wapo vijana waliopata nasafi za utumishi katika madaraja mbalimbali kwa muda mfupi wakawa na maono ya kuwa viongozi wajuu kabisa katika Nchi,
Wenye maono wakishayapata huanza kuyawekeza kwa jamii, kwa kufanya kazi ionekane kwa jamii ili kesho atakaposimama jukwaani kutaka  kuchaguliwa wawakumbushe wananchi kazi wananchi wanaweza kuitolea ushuhuda.

Vijana wenye vipawa vya uongozi na maono huonekana wazi kabisa namna wanavyopigania uwajibikaji, uwazi, na utendaji wa wanaowaongoza
Kijana mwenye uwezo aliyepata nafasi ya kuonekana katika miaka kumi ana uwezo wa kujaza ushuhuda kuliko mzee wa umri wa miaka 50+ aliyejaza mapesa bank kwa ajili ya kufanyia hamasa za kisiasa zisizo na ushuhuda wa kiutendaji.

Hoja au dhana ya umri katika nafasi hii ni mashaka ya watu kwa kijana kwa sababu  hawana historia yake ya kiutendaji, lakini kijana mweye historia ya kiuongozi hata ya miaka 10 tu tena mwenye maono anayejipambanua ana uwezo wa kuongoza taifa kuliko mzee anaedharau vijana kwa sababu ya umri tu.

Naomba nihitimishe kwa ushauri wa bure kwa watu wanaoogopa kumpa kijana nafasi ya urais kwa hofu ya mambo ya ujana wake, wanatoa mifano ya kuwa kijana akiwa rais atajaza warembo ikulu,

Swala la uzinzi ni hulka ya Mtu  wala haijalishi umri wa Mtu, wapo vijana wenye wake zao na hawana mpango wa kwenda nje ya ndoa, lakini wapo wazee wenye familia zao huku wakiwa na Nyumba ndogo tele na watoto wa nje ya ndoa tele,
Kwa hili swala la uasherati umri usitumike kuwasingizia vijana huku tukisahau wazee tele wanakesha disco na wanazijua clubs nyingi kuliko hata vijana.

Sio wazee wote wanaofaa kuwa rais na sio vijana wote wasiofaa kuwa rais

No comments :

Post a Comment

 
Copyright © 2013. BongoAfrica - All Rights Reserved.